Wabunge wamrarua Waziri wa Fedha
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu, akizungumza na wabunge wenzake baada ya kurudi bungeni akitoka kutumikia
adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge mjini Dodoma jana.
Na Bakari Kimwanga, DODOMA
WABUNGE
jana waliendelea kuchachamaa dhidi ya mawaziri na kusema kuwa Serikali ya Rais
Dk. John Magufuli imekuwa na matumizi makubwa kuliko kile kinachopatikana, huku
wakimtaja Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwa ana kiburi na
hashauriki.
Wakati
wabunge mbalimbali wakiendelea kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya
Taifa kwa mwaka 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti, Mbunge wa
Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameibua bomu jipya kuhusu matumizi
ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na kusema kuwa kuna tofauti ya Sh
bilioni 78 za malipo ya mishahara ya watumishi katika kipindi cha mwaka mmoja.
Wakati
Zitto akisema hayo, Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema licha
ya mipango ya maendeleo kupangwa na Bunge, lakini huenda ikakwama kutokana na
kile alichokiita kiburi cha Waziri Dk. Mpango.
ZITTO
Zitto
alisema kuwa pamoja na nia nzuri ya Serikali kubana matumizi, bado kuna ukakasi
kwenye taarifa yake kuhusu matumizi ya fedha za mishahara kwa watumishi.
“Gharama
za watumishi zinazotolewa kila mwezi na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora,
Angella Kairuki pamoja na zile za Benki Kuu (BoT) zinaonyesha kuanzia Agosti
2014 hadi Juni 2015 Serikali ililipa shilingi bilioni 456. Lakini pia
ukiangalia taarifa za hadi Juni 2016 fedha zilizolipwa ni shilingi bilioni 534,
tofauti ikiwa ni shilingi bilioni 18.
“Wakati
Waziri Kairuki akisema katika taarifa zake kuwa wanaokoa shilingi bilioni 19 za
watumishi hewa, ukichukua hesabu zote hizo kwa kipindi hiki utakuta Serikali imetumia
zaidi ya shilingi bilioni 78. Sasa sijui nani mkweli kati ya waziri au BoT,
hivyo kuna mmoja wao anadanganya umma, ni lazima utolewe ufafanuzi wa kina
katika hili. Je, inakuwaje matumizi yawe juu zaidi wakati hakuna ajira mpya?”
alisema Zitto na kuhoji.
Kuhusu
sekta ya elimu ya juu nchini, mbunge huyo alisema ni jambo la kusikitisha kwa
kipindi cha mwaka wa masomo 2017/18 wanafunzi waliokuwa na sifa za kupata
mikopo ya Serikali ni 65,000 lakini waliopata ni 20,000 tu huku wengine
wakikosa.
Zitto
ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, aliponda hatua ya Serikali
kutoa mkopo wa elimu ya juu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi tu na
kuziacha fani nyingine.
Alisema
nchi haiwezi kujengwa na wataalamu wa sayansi pekee, kwamba ni lazima Serikali
iwe na utaratibu wa kufadhili masomo yote ya elimu ya juu ili wataalamu wa fani
nyingine wapatikane pia.
“Huwezi
kujenga uchumi wa viwanda kwa wanasayansi pekee. Je, hivi utakuwa na kiwanda
kwa wanasayansi pekee bila kuwa na watu wa HR (wataalamu wa rasilimali watu),
wahasibu na fani nyingine.
“Ili
tuweze kufika huku, tuwe na utaratibu wa kutoa na ‘scholarship’ kwenye fani
mbalimbali, na hili suala tulilijadili kwenye kamati kutwa nzima na Waziri
Ndalichako (Profesa Joyce) alikuwepo,” alisema.
Zitto
alisema anashangazwa na hatua ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango
kushindwa kusimamia andiko lake lililochapishwa katika jarida la Repoa, kuhusu
hali ya umaskini, ikiwamo kile alichoshauri kuhusu uongozi na timu ya ushindi.
“Ili
kulitekeleza hilo, ni lazima tuwe pamoja. Lakini sasa Serikali na Bunge hawako
pamoja katika mikakati ya uendelezaji nchi. Serikalini mawaziri hawaelewani,
ndiyo maana kila kukicha utasikia matamko na kutengeneza front pages (kurasa za
mbele) za magazeti. Wabunge na Serikali tujichanganye maana sijui wapi
tunakwenda,” alisema.
CHEGENI
Kwa
upande wake, Mbunge wa Busega, Dk. Chegeni, alisema pamoja na utalaamu alionao
Waziri Dk. Mpango, lakini ili afanikiwe lazima aondoe kile alichokiita kiburi.
“Chukua
mawazo ya wabunge fanyia kazi, haiwezekani tupange mipango kwenye kitabu,
lakini utekelezaji wake hatuambiwi iliyopita ikoje na wapi tumekwama.
“Ninajua
Rais Magufuli ana nia njema na Watanzania, haiwezekani mawaziri kuwa na lugha
tofauti. Kupitia mpango huu fanyia kazi hali ya uchumi, mzunguko wa fedha haupo
mitaani na pia hata masilahi yetu wabunge yabebe.
“Rais
anafanya juhudi kubwa ili Watanzania wanufaike na rasilimali zao, nanyi
(mawaziri) msaaidieni, acheni kusigana,” alisema.
HECHE
Naye
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema kuwa uchumi wa nchi
hauwezi kwenda kwa maneno kwani anaona baada ya kutumbuliwa kwa aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga atakayefuata ni Dk. Mpango.
Heche
alisema nchi haiwezi kwenda bila kuwekeza kwenye elimu, lakini kinachofanywa
sasa na Serikali ni kuwatesa wanafunzi wa elimu ya juu.
Alisema
anashangazwa na mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano kutoa kauli za kuwataka
vijana wakajiajiri, huku wao ambao wengine ni maprofesa, madaktari na
hata wanasiasa wa kawaida wamekimbilia kuomba ajira za wananchi.
“Ninashangaa
sana kila siku mnasema vijana mjiajiri, watajiajiri vipi? Na kama nyepesi mbona
wewe umekimbilia huku? Tena wengine ni maprofesa na madaktari. Tena na mama
Ndalichako (Joyce) nilikuwa na kuheshimu kweli ulipokuwa pale Baraza la Taifa
la Mitihani (NECTA) ukionyesha wanafunzi waliochora zombie, lakini leo wewe
ndiyo umechora zombi kubwa ambalo halijapata kutokea.
“Kuna
mwingine mnamwita ‘Mzee wa Sound’, ukimsalimia anaweka mikono mifukoni
anakuuliza unataka kiwanda? Sijui hicho kiwanda amekiweka mfukoni,” alisema
Heche
Comments
Post a Comment