Mahakama za kimila ‘Dagashida’ zatesa walimu
MAHAKAMA za kimila, maarufu kwa jina la Dagashida, zinazoendeshwa na wazee wa kimila maeneo ya vijijini mkoani Simiyu, zimeendelea kuwa mwiba mkali kwa wafanyakazi, hasa walimu kutokana na kuchapwa viboko hadharani. Mfumo wa Dagashida umekuwa ukitumiwa na viongozi wa kimila katika maeneo mengi mkoani Simiyu kuadhibu wananchi, hususani watumishi wa umma, kwa kuwalipisha faini ya fedha, mazao, wanyama na kuchapwa viboko pale wanapoonekana kwenda kinyume na matakwa yao ya kimila, ingawa wakati mwingine wamekuwa wakizushiwa. Mbali na walimu, wafanyakazi wengine ambao wameendelea kuonja joto la mahakama hizo ni wafanyakazi wa Idara ya Afya katika zahanati na vituo vya afya, watendaji wa vijiji pamoja na kata. Mahakama hizo, zinadaiwa kutoa adhabu kali kwa wafanyakazi hao, ikiwemo kuchapwa viboko mbele ya wananchi na wanafunzi, kutengwa pamoja na kutozwa faini kubwa kwa makosa mbalimbali wanayokutwa nayo watuhumiwa. Kutokana na mahakama hiyo kuendelea kujichukulia sheria mkon...