AKIFANYA HIVI SI KWAMBA HAKUPENDI, TAZAMA WAKATI
KUNA wale walio katika ndoa na wale ambao bado hawajaingia katika hatua hiyo. Kwa wale walio katika ndoa huweza kuitwa kuwa wako katika mahusiano halali tofauti na wale ambao bado.
Uhalali wao unakuja kutokana wako huru kutembea pamoja kutambulishana kila mahali na kufanya mengi ambayo wale ambao hawajaoana hawawezi kuyafanya au hata wakiyafanya basi huwa si katika misingi inayokubalika kimaadili na miongozo ya dini zao.
Asilimia sitini ya wakazi wa Tanzania ni vijana na si ajabu kukuta wengi kati yao bado hawajaingia katika ndoa. Ila japo wengi wanaweza kuwa wanasubiri kuingia katika ndoa ila pia si ajabu kukuta asilimia kubwa wana wachumba au wapenzi ambao wako katika harakati za kuingia katika maisha ya ndoa. Kwa wale walio katika hatua madhubuti za kuingia katika ndoa hongereni sana. Na ninaungana nao katika kumuomba Mungu awafanyie wepesi kufanikisha malengo yao.
Ila mbali na hivyo sote tunajua kuwa tupo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Na si ajabu kuna vijana wengine wa Kiislamu wana wachumba wa Kikristo kwa sababu wanaweza kuwa na mipango ya kubadili dini na kuingia rasmi katika maisha ya ndoa. Lengo si kujadili mwezi mtukufu wala dini. Ila lengo ni kuongea kuhusu mabadiliko ambayo huwa ni lazima kutokea katika mwenzi huu.
Mchumba wako anakupigia simu mara ngapi? Mnaonana mara ngapi? Huenda ikawa mara nyingi zaidi ya ninavyoweza kuhisi. Ila kwa vyovyote iwavyo, ndani ya mwezi huu anaweza asikupigie simu wala kukutumia ‘sms’ na wala haina maana kuwa kakuacha na hataki kukuoa tena. Ila anaweza kufanya hivyo kutokana na misingi na mafundisho ya imani yake inavyomtaka.
Katika mwezi huu si ruhusa kuongea au kugusana kimakusudi na msichana/ mwanaume uliye na hisia naye za kimapenzi (kama bado hamjaingia katika ndoa). Na atakayefanya hivi huwa ni sawa na kashinda njaa. Kwa kijana wa Kiislamu aliyekulia madrasa hawezi kuruhusu hali hii. Cha kufanya hawezi kuwa kama zamani.
Yale mazungumzo yatakoma, zile simu zitakatika katika kipindi chote. Yote atakayofanya si kwa kuwa ameghairi kukuoa ila kwa kuwa hataki kubatilisha swaumu yake. Na wewe uliye na mchumba Mwislamu na huenda una mpango wa siku moja kuoana na yeye acha kumuingiza mwenzako katika vishawishi.
Ni vyema katika kipindi hiki ukawa mvumilivu na kutohitaji yale mazungumzo ambayo mlikuwa mnafanya pamoja. Nafahamu kuna wengi watashtushwa na mabadiliko yatakayotokea ila wanapaswa kujua wenzao wapo katika ibada. Suala la msingi ni kuendeleza heshima na nidhamu madhubuti kwa ajili ya mahusiano yao ya baadaye katika ndoa.
Kila imani huwa na masharti yake. Katika imani yako unaweza kusema mnaruhusiwa kufanya hivi ila akikwambia hawaruhusiwi kufanya hivi usilaumu wala kusema mbona sisi tunaruhusiwa! Tambua utofauti huo ndiyo sababu ya imani zenu kuwa tofauti.
Upendo wake kwako hauwezi kumalizwa na ukimya wa mwezi mmoja tu, hapana. Ikiwa kila mmoja ana malengo ya kweli kwa mwenzake wanaweza kuvumiliana bila tatizo. Ila kama mwenzako alikuwa na wewe kwa sababu ya starehe na ‘kuenjoy tu’, muda huu wa mwezi mmoja utakuwa sawa na miaka kumi.
Kwa kuwa una imani kuwa mwenzako anakupenda na yuko katika ibada ndiyo maana kuna ukimya, suala ni kutafakari mambo mengine huku ukijua katika mwezi huu hupaswi kuwa na hali ya mashaka. Kwa maana yuko katika mfungo ambao si tu unamzuia kula na kunywa ila pia unamzuia kusengenya, kuongopa, kutongoza mpaka hilo kubwa unalohofia. Kusaliti!
Kama unavyoamini mapenzi ni sehemu ya maisha pia dini ni sehemu muhimu ya maisha. Hivyo kuacha kuwasiliana naye kwa mwezi mmoja kwa ajili ya kutumikia dini yake si suala baya ila ni zuri zaidi na linaloonesha ni kwa kiwango gani unavyomjali mwenzako katika namna nyingi. Kuwa mvumilivu, omba Mungu awafanyie wepesi muwahi kuingia katika ndoa ili mambo mengi baina yenu yaondokwe na vikwazo. Mfungo mwema kwa wote waliojaliwa. RAMADHAN KAREEM
Comments
Post a Comment