Vyama vingine viige mfano huu wa CCM



PAMOJA na kwamba Tanzania iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni miongoni mwa vyama vikongwe barani Afrika vinavyoendelea kushika dola kwa kutumia uchaguzi huru na haki kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya vyama vingi.
Kwa sasa Tanzania kuna vyama 22 vya siasa vinavyotambulika kisheria na kufanya shughuli zake za kisiasa nchini. Uwepo wa vyama hivyo, umechangia kwa kiasi kikubwa kukuza demokrasia nchini pamoja na kutoa msukumo mkubwa katika suala zima la maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, kumekuwa na changamoto kubwa inayovikabili vyama vingi vya siasa nchini na Afrika kwa ujumla, linapokuja suala la kupokezana vijiti katika uongozi wa ndani wa vyama hicho, kiasi cha kusababisha vyama vingine kujigawa kimakundi au kuingia katika mgogoro mkubwa na wanachama wake.
Vipo vyama vya siasa vinavyofanya vizuri kwa maana ya kujijengea heshima na mvuto miongoni mwa jamii, ikiwemo kuzoa wafuasi wengi kutokana na sera na malengo yake, lakini linapokuja suala la kubadilishana nafasi ya juu ya uongozi vyama hivyo hujikuta vikiharibu.
Kutokana na ukweli huo, imekuwa sasa ni mazoea kwa vyama hivyo vya siasa kuonekana vikiwa na aina ile ile ya viongozi tangu vianzishwe na kinachobadilika ni uongozi wa chini pekee.
Hali hiyo, pia imeonekana hata katika nafasi za juu za kugombea katika uchaguzi kwani vyama hivyo vya siasa hupenda kusimamisha wagombea wale wale kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kuendelea kung’ang’ania madara bila kutoa nafasi ya mabadiliko kwa wengine.
Najua vyama hivyo, vitakuja na sababu za kwanini vimekuwa na mfumo ule ule wa uongozi na hata wa wagombea lakini bado ukweli unabaki kuwa, aina hiyo ya uendeshaji wa vyama kwa kiasi fulani inachangia kuvifanya vyama hivyo virudi nyumba badala ya kuendelea.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hali imekuwa tofauti kwani chama hicho kimeendelea kuonesha ukongwe wake kwa vitendo kwa kuweka mbele demokrasia na si kuangalia maslahi binafsi ya mtu mmoja.
Mmoja wa waasisi wa chama hicho, Pius Msekwa aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa chama hicho kimekomaa katika siasa kutokana na kujiendesha kama taasisi na si chombo cha mtu binafsi.
Hilo limejidhihirisha kwa vitendo kwani juzi Rais John Magufuli alikabidhiwa nafasi ya uenyekiti na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na hivyo kufikisha idadi ya wenyeviti wa chama hicho kuwa watano tangu kianzishwe miaka 40 iliyopita.
Kubadilishana huko kwa uongozi ni kikatiba na tangu kuanze kutekelezwa mwaka 1990 mpaka leo hakuna kiongozi yeyote wa chama aliyevunja Katiba hiyo.
Mwenyekiti wa kwanza wa CCM alikuwa ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyeshika nafasi hiyo hadi mwaka 1990 na kumkabidhi kijiti Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyemkabidhi kijiti Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyemkabidhi kijiti Kikwete ambaye naye juzi amemkabidhi wadhifa huo Rais Magufuli.
Kama ilivyo katika nafasi ya uenyekiti, chama hicho pia kimejijengea demokrasia ya ndani kwa upande wa wagombea Urais, ambapo kila baada ya miaka 10, husimamisha mgombea mwingine kwa lengo la kupokezana uongozi.
Kwa mtindo huo, chama hicho kimekuwa kikitawala Tanzania chini ya viongozi watano tofauti ambao ni Hayati Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete na sasa Magufuli.
Ukweli ni kwamba ukomavu huo wa kisiasa unapaswa kuigwa na vyama vingine kwa kuhakikisha navyo vinatoa fursa ya watu wengine ama kuongoza vyama hivyo lakini pia kugombea nafasi za juu ili kuvijenga vyama hivyo kuwa na mawazo na uongozi mpya wenye tija.
Huenda kuendelea kuwa na sura zilezile kwenye vyama hivyo vya siasa pia kunachangia kuvifanya visifanye vizuri kwenye siasa kwa kuwa watu wanakuwa ni walewale, mawazo yaleyale na sera zilezile lakini hilo likibadilishwa tunaweza kushuhudia upinzani wenye sura mpya nchini

Comments

Popular posts from this blog

NINI MAANA KIGOLI?. AU BINTI KIGOLI

Mambo 10, ya kumfanya mpenzi wako akupende milele@ Kama uliamini mapenzi pesa... SAHAU