EFL: Chelsea watoka nyuma na kulaza Leicester City
Cesc Fabregas alifunga mabao mawili muda wa ziada na kusaidia Chelsea kujikwamua na kulaza Leicester City katika mechi ya raundi ya tatu Kombe la Ligi (EFL).
Leicester walikuwa wamesalia wachezaji 10 wakati wa kumalizika kwa mechi baada ya Marcin Wasilewski kupewa kadi nyekundu dakika ya 89.
Muda mfupi kabla ya mapumziko, Chelsea walikuwa 2-0 nyuma kutokana na mabao ya Shinji Okazaki dakika ya 17 na 34 lakini Gary Cahill alikomboa moja muda mfupi kabla ya kipenga cha mapumziko kupulizwa.
Cesar Azpilicueta alisawazisha kwa kombora la mbali dakika ya 49.
Fabregas, 29, aliwaweka mbele kwa bao alilofunga dakika ya 92 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 94.
Wasilewski alioneshwa kadi ya pili ya njano kwa kumgonga kwa kiwiko cha mkono mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa.
Leicester watarejea uwanjani Ligi ya Premia kwa mechi ya ugenini dhidi ya Manchester United Jumamosi.
Chelsea, nao watakuwa ugenini Arsenal siku iyo hiyo baada ya kulazwa 2-1 na Liverpool ligini Ijumaa iliyopita
Comments
Post a Comment