Video ya raia wa Uganda akiuwawa na polisi Marekani yatolewa
Polisi katika mji wa Marekani San Diego wametoa mkanda wa video ya mwanamme mweusi aliyepigwa risasi na kuuwawa na polisi siku ya jumanne.
Video hiyo inaonyesha maafisa wawili wa polisi wakimkaribia Alfred Olango - mkimbizi kutoka Uganda - ambaye hakuwa amejihami, kabla ya mmoja wao kumfyatulia risasi katika mtaa wa El Cajon.
Polisi wanasema kwamba mwanamme huyo alionyesha tabia potovu isiyoeleweka, japo mamake mzazi anasema alikuwa na matatizo ya kiakili na alifaa kupata usaidizi.
Tukio hilo lilisababisha maaandamano makali katika eneo la El Cajon.
Polisi huyo anaonekana akifyatua risasi mara nne, baada ya mwanamme huyo kuinua mikono yake hadi kwenye eneo la kifua, ishara ambayo polisi wanasema ilikuwa ya kujitayarisha kufyatua risasi.
Video hiyo imetolewa baada ya siku tatu za maandamano makali , na katika mkesha wa siku ambayo familia ya mwanamme huyo iliitisha maandamano makubwa.
Familia ya mwanamme huyo ilikuwa ikiwashinikiza polisi kutoa mkanda wa video wa tukio hilo.
Mkuu wa polisi Jeff Davis anasema video hiyo imetolewa ili kutuliza ghadhabu ya umma.
Olango, aliye na umri wa miaka 38, mkimbizi kutoka Uganda ambaye ameishi nchini Marekani tangu utotoni, alipigwa risasi baada ya polisi kujibu ripoti kuhusu mwanamme aliyekuwa na matatizo ya kiakili, ambaye alikuwa akitembea ovyo barabarani.
Polisi wanasema, Olango, alikataa kuondoa mkono wake kwenye mfuko alipioagizwa, na alifyatuliwa risasi baada ya kuondoa kifaa kwenye mfuko, na kufanya ishara ya kufyatua risasi.
Kulingana na polisi, aliwaelekezea kifaa chenye ncha kali "kana kwamba alikuwa anawafyatulia risasi, japo baadaye ikagunduliwa kifaa hicho kilikuwa cha sigareti ya elektroniki.
Comments
Post a Comment